Uongozi
wa Klabu ya Simba, umetamka wazi kuwa, hautakuwa tayari timu yao
kucheza mechi yoyote dhidi ya watani zao wa jadi, Yanga huku waamuzi
wakiwa ni Watanzania.
Kauli
hiyo imetolewa leo na Mkuu wa Kitengo cha Habari na Mawasiliano wa
Simba, Haji Manara wakati akiongea na waandishi wa habari katika makao
makuu ya klabu hiyo, Kariakoo jijini Dar.
Manara
alisema sababu kubwa ya kufanya hivyo ni kutokana na kila wanapokutana
na Yanga kuonewa kwa makusudi na waamuzi ambao wanaonesha dhahiri kwamba
wametumwa, hivyo wamechoka kuonewa, sasa wanataka haki itendeke kwa
kuchezeshwa na waamuzi kutoka nje.
“Tumecheza
na Yanga mara nyingi tu, na mchezo wetu wa mwisho wa ligi kuu tulitoka
sare ya bao 1-1, lakini mwamuzi wa kati siku ile, Martin Saanya
alionekana dhahiri kutunyonga.
“Matukio
ni mengi ya kustaajabisha yalitokea ikiwemo kulikataa bao letu halali
na kulikubali la Yanga ambalo mfungaji kabla ya kufunga, aliukumbatia
mpira kama mtoto, kisha akafunga, halafu mwamuzi eti anaita kati
kuashiria bao.
“Haitoshi,
wachezaji wetu wanalalamika, anakuja kumuadhibu nahodha wetu, Jonas
Mkude kwa kumpa kadi nyekundu ya moja kwa moja, lakini kwa kuwa Mungu
hamtupi mja wake, ile kadi ikaja kufutwa na Kamati ya Saa 72 ambayo
iliona mwamuzi wao kachemsha.
“Kwa hali hii, hatutakuwa radhi kuingiza timu uwanjani endapo tu waamuzi wakiwa ni walewale. Tumechoka kuonewa,” alisema Manara.
Katika
kukazia hilo, Manara alisema wapo radhi wao kama Simba, mapato yote ya
mchezo wao dhidi ya Yanga wagharamie kila kitu kwa waamuzi hao wa nje
ili waje wasimamie haki.
“Tutagharamia
kila kitu kwa ajili ya waamuzi kutoka nje, hata mapato yetu yote ya
mchezo tutatoa kwani tunataka haki itendeke, mbona nchi za wenzetu kama
Misri wao wanaweza kufanya hivyo kwa mechi kubwa kama yetu hii, kwa nini
sisi tushindwe,” alisema.
Aidha
Manara alisema kutokana na Simba kuonewa mara kwa mara, kamati ya
utendaji ya klabu hiyo, imefikia makubaliano ya kumuandikia barua Rais
wa Shirikisho la Soka Tanzania (TF), Jamal Malinzi ili wakutane waongee
ni kwa nini klabu yao imekuwa ikionewa kila kukicha.
“Tumemwandikia
barua Malinzi ya kumtaka tukae tuzungumze tuone Simba ina tatizo gani
mpaka iwe inaonewa kila siku, tunataka tulifahamu hilo ili kuondoa hali
hii ambayo sasa imetuchosha,” alisema Manara na kuongeza.
“Tumeitisha
mkutano wetu wa wanachama kwa ajili ya mabadiliko ya katiba, halafu
tunasikia kuna mtu huyu anajiita Mohammed Kiganja (Katibu wa BMT) eti
anasema kitakachoafikiwa siku hiyo wao hawakitambui wakati waziri
mwenyewe amekubali.
“Sasa
huyu Kiganja ni nani hasa mpaka atuendeshe kiasi hiki, sisi tunasema,
katika hili hakuna wa kutuzuia, tutafanya mabadiliko ya katiba kama
wanachama wakikubali, hakuna wa kutuingia katika katiba yetu hata kama
serikali ilihali hatuvunji katiba ya nchi.
“Hivi
kwa soka la sasa ni nani asiyependa mabadiliko, huyu Kiganja yeye
amekuwa akijitokeza kwenye migogoro tu, kwa nini katika maendeleo
hayupo, tumefuata sheria zote za kuitisha mkutano na tutaufanya bila ya
kizuizi chochote kile,” alimaliza Manara.
0 comments :
Post a Comment