Kiungo nyota wa Yanga, Haruna Niyonzima, amesema kuwa, timu yao kwa sasa siyo ya kuibeza kutokana na mazoezi na maandalizi wanayoyafanya chini ya kocha, George Lwandamina hivyo wamejipanga kutembeza kichapo kwa kila timu watakayokutana nayo mzunguko wa pili.
Yanga juzi ilikumbana na kichapo cha mabao 2-0 kutoka kwa JKU katika mchezo wa kirafiki kwenye Uwanja wa Uhuru jijini Dar lakini kocha George Lwandamina akabeza kwa kutamka kuwa ilikuwa ni mechi yake ya kuangalia wachezaji alionao tu.
Yanga ilimaliza mzunguko wa kwanza ikiwa nafasi ya pili ya msimamo wa ligi kwa kuwa na pointi 33 nyuma ya Simba yenye pointi 35. Ilikuwa chini ya Mholanzi, Hans van Der Pluijm lakini sasa ipo chini ya Mzambia Lwandamina na Pluijm amesukumwa hadi kwenye ukurugenzi wa benchi la ufundi.
Niyonzima amesema wamejipanga kutembeza kichapo kwa kila timu wakiwemo mahasimu wao Simba mzunguko wa pili ili waweze kufanikiwa kutetea ubingwa wao.
“Tumejiandaa vizuri kwa ajili ya mzunguko wa pili wa ligi, ni kweli Simba wametupita pointi mbili lakini sisi hatuziangalii hizo na kitu tunachokiangalia hivi sasa ni kuhakikisha tunafanikiwa kuifunga kila timu katika mzunguko wa pili.
“Tunahitaji kutetea ubingwa wetu kwani maandalizi na mazoezi tunayoyafanya chini ya kocha wetu Lwandamina si ya kitoto, kila mchezaji anaonyesha kujituma na kujiamini zaidi.
“Malengo yetu ni kuona tunafanikiwa kufanya vizuri kwenye ligi na michuano ya kimataifa kwani kuna ushindani wa hali ya juu na tunahitaji kufika mbali zaidi ya mwanzo hatua ya makundi,” alisema Niyonzima.
0 comments :
Post a Comment